|
|
|
|
Maumivu ya ukimya
“Nilipatikana na virusi vya UKIMWI mwaka 1997 nilipokuwa najitayarisha kwenda kwa masomo ya juu huko Ulaya,” anasema James, kijana mmoja mfanyakazi wa Benki moja iliyopo Dar es Salaam.
Matokeo hayo yalimfadhaisha sana kiasi kwamba ingawa alikuwa na mdhamini wa kumlipia gharama za masomo hayo aliachana na mpango wa kuendelea nayo.
“Nilifadhaika, kusema kweli, sidhani kama kuna mtu atakayegundua kuwa ana virusi vya UKIMWI na asipate hisia kali za aibu, ghadhabu na woga,” anasema James (si jina lake halisi).
Nilipokuwa mwanafunzi nilikuwa na wasichana wengi na sikuwa mwangalifu sana. Mwanzoni nilifikiria nimepewa adhabu ya kifo. Sikujua nitaishi kwa muda gani, nilijisikia sina maana, kama mtu aliyeshindwa na maisha na kuwa ni aibu kwa familia yangu. Hakuweza kumwambia mtu yeyote katika familia yangu.
BAADA YA KIMYA CHA MIAKA, JAMES AIAMBIA FAMILIA YAKE James amepata jinsi ya kuishi na ugonjwa huo. Anajitokeza akiwa mcheshi, mtu anayejiamini, tofauti na mtu anavyoweza kudhania. “Nimeshauriwa sana na baadhi ya taasisi kama CCBRT, WAMATA, PASADA na SWAT. Hii imekuwa muhimu kwangu. Kuweza kukutana na kuzungumza na wengine ambao wana virusi, kumenifariji sana na kunipunguzia mzigo, kujiona mpweke, mwenye kujawa na hofu na kukata tamaa. Kadri muda unavyopita nimeanza kukubaliana na ukweli na kuepukana na hali ya kujihurumia.”
Nimejifunza mengi kuhusu UKIMWI na virusi vyake na jinsi ya kuishi vizuri na virusi hivyo. Amebadili mambo mengi katika maisha yake, anautunza mwili wake kwa kula vyakula vyenye lishe ambavyo vinamuongezea kinga, anatibu ugonjwa wowote anaopata na anapumzika muda mrefu kuepuka uchovu. Anaishi maisha yake vizuri tena, akijishughulisha zaidi na kazi yake ya benki, ambayo anaiona inampa changamoto. Zaidi ya hayo, ana rafiki wa kike na mpenzi katika maisha yake. “Nilikuwa wazi kwake kuhusu hali yangu. Alikubali kupimwa, lakini akaonekana hana ugonjwa. Licha ya matokeo hayo, akaamua asinikatae bali tuendelee na uhusiano wetu, yeye ni mtu maalum sana kwangu,” anasema James.
ANAENDELEA KUPATA USHAURI NASAHA Aidha James anasema kwamba anaendelea kupata ushauri nasaha na anajihadhari kwa kujamiiana kwa kutumia kondom. “Sitaki apate virusi na kama tukiwa waangalifu hatapata. “Anashirikiana naye kwa kila kitu, anamsaidia na anamwelewa kwa undani zaidi. Nina bahati kuwa na mtu kama yeye, anayenifanya nisibebe mzigo huu peke yangu”.
James anasema Kuishinda hofu, usiri na kukataliwa kutokana na ukimwi katika jamii yetu, ni jambo gumu kukabiliana nalo. James bado hajakuwa na dalili zozote za UKIMWI na hadi sasa hajawaambia ndugu na marafiki zake kuwa ana virusi vya UKIMWI. “Naogopa kwamba hawatanielewa na nataka nisimtie mama yangu hofu na kumkatisha tamaa. Kila mtu ataniteta na kunisema vibaya mimi na familia yangu, na baadhi yao watanikataa kwa kuwaletea aibu”.
NI VIBAYA WAATHIRIKA KUTOZIAMBIA FAMILIA ZAO James anaamini kwamba ni vibaya kwa walioathirika kutowaambia wanafamilia wao, lakini kuwa na virusi vya UKIMWIi hapa Tanzania kunamwonyesha aliyembukizwa kuwa mzinzi na mara nyingine unachukiwa. “Sitaki kupewa upendeleo kwa kuwa nina virusi, nataka nifanyiwe kama mtu mwingine yeyote”. James pia anaogopa kueleza kazini kama ana virusi, kwa kuwa anaamini itasababisha abaguliwe. “Wenzako hawatakuhusisha katika masuala ya maendeleo kwa sababu wanafikiri utakufa leo au kesho. Hivyo naficha siri yangu, lakini inanifanya nijione naishi maisha ya kujidanganya, kwa kujifanya mimi ni mtu mwingine”.
James anafikri ubaguzi dhidi ya wenye virusi, mtazamo na doa linaloambatana na hali hiyo, inachangia kuenea kwa virusi hivyo. “Hali ya kukataliwa inaongeza madhara, nafikiri kama watu wanaoishi na ukimwi wangetendewa vizuri na kuhusishwa katika mapambano dhidi ya kuenezwa kwa virusi, tungeona mabadiliko,” anasisitiza. “Ni wakati wa kuchukua hatua, ili watu waanze kuzungumza waziwazi kuhusu ugonjwa huo. VVU/UKIMWI sio suala la mtu binafsi; linahusu jamii yote, na maendeleo ya nchi yetu. Kizazi kizima cha vijana wenye uwezo kama mimi ambao wanastahili kujenga nchi yetu, wameambukizwa.”
UJUMBE WA JAMES KWA VIJANA Wote mnajua kuhusu VVU/UKIMWI. Tafuta habari zaidi. Jihadhari. Kuwa mjanja zaidi kuliko nilivyokuwa mimi, fanya uamuzi sahihi. Chaguo ni lako, SUBIRI kujamiana hadi unapokuwa mkubwa kiumri ama tumia KONDOM. Lazima tufanye juhudi kupunguza hofu ya virusi na UKIMWI na kuwafanya watu kuwa na matumaini ya hali ya baadaye.
Mchango wako ni mkubwa katika kuzuia maambukizo.
| |
 |
 |
 |
Unafikiri nini kuhusu makala hii? Tupe maoni yako
hapa >> |
 |
 |
» to Top of article
»Back to List
|
|
|
|