Logo
Sera ya Lugha kiengerezi

Unyanyapaa
Haki za Walioathirika
Zaidi
Niende wapi
Stori yangu
 Maswali na Majibu
Chagua Lugha
Kuingia katika majadiliano

 
   
   Hujaandikishwa?
   Andikisha
hapa

   Homepage > VVU/UKIMWI > Kuishi kwa matumaini > Maswali na Majibu
Maswali na Majibu

Chagua swali hapa chini kuona jibu lake!

Kama umeshaambukizwa na ukianza kutumia dawa za kurefusha maisha utaishi kwa muda gani zaidi?
Kwanini wajane huishi muda mrefu sana baada ya waume zao kufa kwa UKIMWI?
Je, tuwatenge waliokwishaambukizwa virusi vya UKIMWI?
Kama mwathirika anaweza kuishi miaka mingi, kwanini matangazo kuhusu UKIMWI hutilia kifo msisitizo?
Kwanini serikali isiwatenge waathirika ili wasiendelee kuambukiza wengine?
Kwanini serikali isiwatangaze hadharani waliokufa kwa UKIMWI?
Dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV) ni nini?
Mama yangu ana maambukizo ya virusi vya UKIMWI na yuko wazi kusema

Kama umeshaambukizwa na ukianza kutumia dawa za kurefusha maisha utaishi kwa muda gani zaidi?
Muda utakaoongezeka unatofautiana kati ya mtu na mtu kuendana na:

-Hali ya mtu wakati anaanza matibabu
-Uwezo wa kufuata masharti ambayo ni:
-Kutumia dawa kwa kufuata ratiba bila kukosa
-Kujitunza, kula kwa kufuata kanuni za afya
-Kuwahi kutibiwa magonjwa nyemelezi mapema

Kwanini wajane huishi muda mrefu sana baada ya waume zao kufa kwa UKIMWI?
Muda wa kuishi tangu kuathirika unatofautiana kati ya mtu na mtu. Wako wanaoishi muda mfupi, kiasi au mrefu kutokana na mambo kadha wa kadha kama vile lishe bora, kujitunza, kutibiwa maradhi na kujijali katika mambo yote ya kimwili. Yawezekana wajane hawa wakaishi muda mrefu kwa kuzifuata kanuni bora za kuishi na VVU.

Je, tuwatenge waliokwishaambukizwa virusi vya UKIMWI?
Watu wenye UKIMWI ni binadamu na wana haki kama binadamu wengine. Watu hawa wanahitaji misaada na mawazo yetu. Mila na desturi zetu tangu awali hazitengi watu wenye matatizo kiafya bali huwatunza na kuwapa msaada. Hivyo, kuwatenga watu wenye UKIMWI ni ishara ya kuvunja familia na kuleta taabu nyingi katika jamii.

Pia kitendo hicho, kitalipunguzia taifa letu nguvu kazi yenye kutegemewa kwa kuwa baadhi ya watu wenye UKIMWI bado ni hazina kwani wana utaalamu katika nyanja mbalimbali. Vilevile, bado wanahitajika katika familia zao n.k.

Kama mwathirika anaweza kuishi miaka mingi, kwanini matangazo kuhusu UKIMWI hutilia kifo msisitizo?
Ni bahati mbaya, kampeni nyingi husisitizia kwamba anayeathirika hufa. Kampeni za namna hii huimarisha unyanyapaa. Ni vema matangazo haya yakaonyesha pande zote mbili, yaani waathirika wenye afya nzuri na waathirika wenye hali isiyo ya kuridhisha

Kwanini serikali isiwatenge waathirika ili wasiendelee kuambukiza wengine?
Haki za binadamu za kimataifa na kitaifa zinawalinda waathirika na familia zao na serikali haiwezi kuingilia kati.
•Wasinyanyapaliwe wala kutengwa.
•Hata hivyo nani atengwe na nani asitengwe?
•Tungelipima wote na kuwa wazi bado tungeendelea kuishi pamoja.

Kuwatenga waathirika siyo njia sahihi ya kuzuia usambazaji wa VVU
Jambo la msingi ni kutoa elimu ya kutosha ili wasieneze VVU.

Kwanini serikali isiwatangaze hadharani waliokufa kwa UKIMWI?
Haki za binadamu zinawalinda hata waliokufa. Hasara za kutangaza ni kubwa kuliko faida za kutangaza. Hata kama serikali ingetangaza, watakaopata taarifa ni wale waliopo kwenye mazishi. Yawezekana matangazo haya yasifike kule walikopatia maambukizi/alipokuwa anaishi. Na tujiulize matangazo haya yatamsaidia nani saa hizi?

La msingi ni kuwa elimu ya kutosha itolewa, hakuna haja ya kutangaza. Jilinde na uwalinde wengine.

Dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV) ni nini?
SWALI KAMILI (katika mfumo wa barua kwa Shangazi Stella):

Mpendwa Shangazi Stella
Mimi nina umri wa miaka 19 na nina mtoto wa kike
mwenye umri wa miaka 3. Rafiki yangu wa kiume
niliyezaa naye alikuwa mkubwa kwangu na aliniacha
nilipopata mimba tu. Sasa hivi anaumwa sana, na ana
UKIMWI. Mimi ninaishi kijijini na bibi yangu. Msimu wa
mvua tunalima mahindi.Vilevile, tunafanya biashara ya
kuuza samaki wakavu. Hata hivyo pesa hazitoshi.Afya
yangu ni nzuri. Lakini mwaka jana nilianza kupungua
uzito na mara nyingine kujisikia dhaifu na kuchoka.
Miezi michache iliyopita Shangazi yangu alinipeleka
kliniki ili nikapime kama nina maambukizo ya VVU.
Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kufahamu kwamba
ninayo maambukizo ya VVU.
Mama mmoja huko katika nyumba ya kufanyia ibada
aliniambia kuwa zipo dawa za kupunguza makali ya
VVU lakini ni ghali sana. Pamoja na hayo ningependa
kupata dawa hizo.Wasiwasi wangu mkubwa ni mtoto
wangu. Nani atamtunza mimi nikifa? Bibi yangu ni
mzee sana na wakati mwingine anakuwa mgonjwa.
Ninataka kumwona mtoto wangu akienda shuleni na
vilevile anakuwa na furaha.
Tafadhali Shangazi naomba uniambie iwapo kuna
mahali ambapo ninaweza kuzipata dawa hizi.

Tedy

JIBU (pia kama barua):

Mpendwa Tedy

Dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) ni dawa ambazo
zinaweza kuwasaidia watu ambao wana UKIMWI.VVU haviondoki
lakini dawa husaidia visiendelee kuzaliana, hivyo kuruhusu
kuongezeka kwa kinga ya mwili. Ni kweli dawa hizi ni ghali. Lakini
bei sasa hivi zimepungua kidogo. Vilevile, Serikali inatoa bure.
Hata hivyo, dawa hizi zina nguvu sana na hazieleweki vizuri, kwa
kawaida watu huanza kuzitumia wanapokuwa wagonjwa sana.
Kamwe usitumie dawa hizi bila ya kupima na kupata ushauri
kutoka kwa daktari. Unatakiwa kujihakikishia kwamba unao uwezo
wa kuzinunua kipindi chote cha maisha yako kwa sababu ni hatari
kuanza kuzitumia halafu unaacha katikati na kurudia tena.
Kumbuka vilevile kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU si njia
pekee ya kuwa na afya. Afya inaweza kurudia hali ya kawaida kwa
kula chakula sahihi, kupata vitamini na kuishi kwa matumaini. Hii ni
pamoja na kutibu magonjwa nyemelezi mapema.
Dawa za kupunguza makali ya VVU hukufanya ujisikie vizuri zaidi
lakini VVU vinakuwepo mwilini mwako, kwa hiyo unaweza
kumwambukiza mtu mwingine au wewe mwenyewe kupata
maambukizi mapya. Kumbuka, kila mara tumia kondomu
unapofanya ngono au fanya ngono salama.
Kama unatumia au hutumii dawa za kupunguza makali ya VVU,
jaribu kuishi maisha ambayo si hatarishi, utakuwa na miaka mingi
ya kumtunza mtoto wako.
Kila la heri

Shangazi Stella

(Huduma kamili za Shangazi Stella zinapatikana kutoka www.auntiestella.org; Kwa wale wanaozungumza Kiswahili pekee, huduma hizi zinapatikana kutoka mradi wa elimu na kujikinga na VVU/UKIMWI kwenye shule za sekondari – PASHA/GTZ)

Mama yangu ana maambukizo ya virusi vya UKIMWI na yuko wazi kusema
SWALI KAMILI (katika mfumo wa barua kwa Shangazi Stella):

Mpendwa Shangazi Stella

Mimi ni mvulana mwenye umri wa miaka 22. Mama yangu anaishi
na VVU na yeye mwenyewe husema hivyo waziwazi. Yeye anafanya
kazi katika shirika moja linaloshughulikia masuala ya UKIMWI.
Mama husema hakuna haja ya kuona aibu kwa sababu ya
VVU/UKIMWI. Yeye husema kwa nini nifiche? Tunaoishi na VVU
tunahitaji upendo kukubalika na kila mtu.
Mama aliponiambia ana maambukizo ya VVU, mimi nilikuwa
ninasoma Darasa la Nne. Mwanzoni niliogopa sana. Nilifikiri mama
yangu angalikufa wakati wowote, lakini sasa hivi ninaelewa kuwa
unaweza kuwa na maambukizo ya VVU na ukaishi kwa muda wa
miaka mingi ukiwa na afya nzuri. Mama ameishi na VVU kwa muda
wa miaka 12 sasa. Anajihudumia kwa kula chakula kizuri na
kupumzika, kwa hiyo mara nyingi afya yake ni nzuri. Mama
anasema tunatakiwa kuwa wawazi kuhusu VVU na UKIMWI na
kuvunja uoga kwa kila mtu ili kila mtu aweze kuwahudumia vizuri
wale wenye maambukizo.
Mimi sikubaliani naye, watu wana mtazamo mbaya kuhusu UKIMWI
kwa hiyo haina maana kuwaeleza. Ndugu wa karibu wanaweza
kuelezwa lakini nao pia itabidi wasiseme kwa watu wengine yaani
iwe siri.
Jambo moja ambalo tunakubaliana ni kuwa, watoto lazima
waelezwe kwa sababu, kwa vyoyote vile watajua tu. Ni muhimu
wafahamu ukweli ili waweze kuzungumzia jambo hilo.
Kwa hiyo Shangazi, wewe unalionaje jambo hili? Ninampenda sana
mama yangu na ninajivunia kuwa naye. Lakini, nani kati yetu ni
sahihi?

Hamisi

JIBU (pia kama barua):

Mpendwa Hamisi

Siwezi kukupatia jibu kuhusu nani umweleze kuwa una
maambukizo ya VVU au UKIMWI, ni uamuzi mzito na ni
mkubwa. Kila mtu lazima afanye uamuzi wake mwenyewe.
Wengine huamua kutomweleza mtu yeyote, wengine
humwambia ndugu wa karibu au rafiki, wengine huwaeleza watu
wengi na hufanya hivyo katika hatua tofauti. Lolote
wanalochagua watu ni sawa tu.
Watu wengi hujisikia kuwa na furaha wanapowashirikisha hisia
zao watu wengine, kama mama yako ni jasiri mno kiasi cha
kuongea hadharani. Na kwa yeyote anayeishi na VVU au
UKIMWI kuwa na mnasihi wa kuzungumza naye au kikundi cha
kutoa msaada ni muhimu sana.
Hata hivyo, mpaka jamii itakapokuwa wazi kuhusu VVU,
kuwaeleza watu una VVU kunaweza kuleta matatizo makubwa
kama vile kupoteza kazi, marafiki au wapenzi au hata mahali pa
kuishi.Watu wanahitaji kupima faida dhidi ya hasara
watakazozipata binafsi kabla ya kumweleza mtu yeyote kwamba
wana maambukizo ya VVU. Iwapo ni mfanyakazi unahitaji kujua
haki zako za kisheria kama mfanyakazi unayeishi na VVU.
Kweli, ninakubaliana na wewe kuwa, kwa kawaida watoto huwa
na furaha zaidi wanapojua ukweli hata kama unahuzunisha.
Kwa hiyo, ninashukuru kwa kuwasaidia vijana wengi kuwa jasiri
na wawazi. Hadithi yako na ya mama yako zitatoa matumaini
kwa watu wengi.

Shangazi Stella

(Huduma kamili za Shangazi Stella zinapatikana kutoka www.auntiestella.org; Kwa wale wanaozungumza Kiswahili pekee, huduma hizi zinapatikana kutoka mradi wa elimu na kujikinga na VVU/UKIMWI kwenye shule za sekondari – PASHA/GTZ)