Chagua swali hapa chini kuona jibu lake!
|
Nifanye nini kama sitaki kujamiiana kabla ya ndoa? |
|
Umri mzuri wa kuoana ni upi? |
|
Je nifanye nini ili mpenzi wangu asiwe na wapenzi wengine? |
|
Kwa nini vijana wanakatazwa kujamiiana? |
|
Je, nifanyeje ili kuhakikisha ninafanya tendo la kujamiiana salama? |
|
Watu wengi wanasema ni vizuri kufahamu tabia ya rafiki yako wa kike/kiume kabla ya kuoana.Nitafahamu vipi kama tunaishi mbalimbali? |
|
Nifanyeje kuepuka vishawishi vya kujamiiana kutoka kwa watu wengine hasa wakubwa? |
|
Je, nitahakikisha vipi kwamba urafiki wetu ni wa kudumu? |
|
Watu hujamiiana ili kutafuta watoto, nini lengo la kujamiiana iwapo huhitaji watoto? |
|
Nani anayevisha kondom kwenye uume? Mwanamke au mwanaume? |
|
Je, nikitumia kondom kila mara ninapojamiiana sitaaambukizwa magonjwa ya zinaa? |
|
Nifanyeje kujiepusha na vishawishi vya mpenzi wangu vinavyoweza kunifanya nisitumie kondom? |
|
Je, nifanye nini ili wazazi wangu wakubaliane na mimi kuhusu mchumba niliyemchagua? |
|
Nikitafuta rafiki kwa nia ya kuoana (mchumba) niangalie sifa gani? |
Nifanye nini kama sitaki kujamiiana kabla ya ndoa?
Kama umeamua kutojamiiana kabla ya ndoa ni uamuzi mzuri na ni haki yako. Kwa kufanya hivyo unaepuka madhara ya kujamiiana katika umri mdogo.
Hakuna haja ya kujisikia vibaya unaposikia vijana wenzako wanapoelezea raha wanayoipata wakati wa kujamiiana. Una haki ya kujisifu kwamba mpaka sasa hivi umeweza kuvumilia kutojamiiana. Kumbuka kwamba vijana wengi wanaozungumzia kujamiiana wanatia chumvi tu.
Iwapo rafiki zako watazidi kukunyanyasa kwa kutokujamiiana, waeleze sababu ya uamuzi wako. Wafafanulie madhara ya kujamiiana katika umri mdogo. Kama wataendelea kukushinikiza kujamiiana achana nao, tafuta marafiki wengine utakaoelewana nao vizuri.
|
Umri mzuri wa kuoana ni upi?
Kabla ya kuoana ni vizuri kujenga msingi mzuri wa maisha na mahusiano kati yenu na kuwa tayari kubeba majukumu ya ndoa. Kuoana maana yake ni kuwajibika kwa maisha yako na mwenzi wako na mara nyingi kunaambatana na kuzaa watoto. Ni vigumu sana kutambua umri sahihi wa mtu kuoa au kuolewa. Wengine wanakuwa tayari katika umri wa miaka 20 na wengine katika umri mkubwa zaidi.
Kwa vile kuoa au kuolewa mara nyingi kunahusishwa na mtu kuanza familia kuna vipengele vya kiafya vinavyofaa kuzingatia. Kwa mfano siyo vizuri kwa msichana kuzaa kabla hajafikisha miaka 18 au 20 kwani mwili wake hauko tayari kubeba mimba. Viungo vyake vya uzazi ni vidogo na laini kiasi ambacho vinaweza kuharibika wakati wa kuzaa mtoto.
Kwa hiyo basi mnashauriwa kusubiri kuoana mpaka hapo mtakapokuwa mmekomaa na mmejenga msingi mzuri wa maisha yenu. Unaweza kuwa na rafiki wa kike/kiume kabla ya kuoana ili taratibu muweze kuelewana tabia; yale anayoyapenda na asiyoyapenda na kujenga msingi mzuri wa mahusiano.
|
Je nifanye nini ili mpenzi wangu asiwe na wapenzi wengine?
Mawasiliano ya karibu hufanya uelewe mawazo na matatizo ya mpenzi wako. Mwonyeshe na mthibitishie kwamba unampenda na huna mwingine zaidi yake. Hakikisha unakuwa muwazi na mkweli. Mkielewana vizuri mnaweza kusaidiana katika kutatua matatizo iwapo mmoja wenu atakuwa nayo. Kwa kufanya hivyo mtajenga moyo wa kuaminiana.
Jitahidi usiwe na marafiki wengine. Utamfahamu vizuri rafiki yako iwapo mtazungumza kila mara kuhusu mipango ya uhusiano wenu, vitu anavyopendelea kufanya baada ya saa za kazi au masomo,watu anaowasiliana nao n.k.
IWAPO HAMTAAMINIANA JIULIZE Kwa nini iwe hivyo. Je, inawezekana huyu mtu hanifai au mapenzi yangu ni kidogo kiasi ambacho siwezi kuzuia vishawishi vingine?
|
Kwa nini vijana wanakatazwa kujamiiana?
Ujana ni kipindi muhimu cha kuweka msingi wa maisha ya baadaye. Matatizo mbalimbali yanaweza kutokea iwapo ukijamiiana na kuharibu msingi huo. Ni kipindi cha mabadiliko kutoka utotoni kuelekea utu uzima. Ni wakati ambao kijana hupata mabadiliko ya kimwili, kiakili na kimtazamo. Mwili na akili hupevuka.
Mimba zisizopangiliwa, kufukuzwa shule na kutengwa na jamii ni baadhi ya matatizo ya kujamiiana katika umri mdogo. Mengine ni ya kiafya. Kwa vile mwili wa msichana unakuwa haujakomaa, unakuwa haujajiandaa kwa uzazi. Pia kutokana na msichana anakuwa bado hajajitegemea kimatumizi inakuwa ni hatari kwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa na UKIMWI kutokana na kujirahisi ili kupata mahitaji.
Kujamiiana katika umri mdogo kunaweza kuleta madhara mengi kwa afya yako na malengo yako maishani. Hivyo basi unapokatazwa kujamiiana ni kwa sababu ya matatizo haya.Hata hivyo, kama kwa vyovyote huwezi kuacha kujamiiana, hakikisha kwamba unajikinga kwa kutumia kondomu.
|
Je, nifanyeje ili kuhakikisha ninafanya tendo la kujamiiana salama?
Mapenzi salama ni yale yanayofanyika bila wasiwasi wa kupata mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa pamoja UKIMWI. Mapenzi salama yanaweza kuwa ni pamoja na kumaliza hamu bila ya kujamiiana. Mapenzi salama pia ni yale yanayohusisha kuchukua tahadhari wakati wa kujamiiana.Kumaliza hamu bila ya kujamiiana ni pamoja na kupiga busu, kukumbatiana, kupiga punyeto. Jambo jingine ni uaminifu katika mapenzi. Ni vizuri wote wawili muwe na uhakika kwamba hamna maambikizi ya magonjwa kabla hamjaanza kujamiiana kwa mara ya kwanza.Mwisho kabisa ni kutumia kondom. Uzuri wa kondom ni kwamba inazuia mimba na magonjwa ya zinaa.
|
Watu wengi wanasema ni vizuri kufahamu tabia ya rafiki yako wa kike/kiume kabla ya kuoana.Nitafahamu vipi kama tunaishi mbalimbali?
Unaweza kufanya uchunguzi wa kutosha kuhusu tabia ya rafiki yako hata kama mnaishi mbalimbali.Unaweza kumuuliza maswali kuhusu mahali anapoishi na familia yake kwa ujumla. Jaribu kufanya mawasiliano ya karibu zaidi ili uweze kumdadisi, na yeye aweze kujieleza mwenyewe kwa undani zaidi kuhusu yeye mwenyewe. Njia nyingine ni kutumia watu wengine walio karibu naye.Unapomchunguza mtu ambaye unafikiri anaweza kuwa mchumba wako inakubidi uwe na vigezo ulivyojiwekea ambavyo ungependa awe navyo.Uchunguzi wa namna hiyo unaweza kukusaidia kujua tabia ya rafiki yako. Hata hivyo kufanya uchunguzi hakuna maana kwamba huhitaji kuwa naye kabisa. Bado unahitaji muda zaidi wa kuwa naye ili kumjua na na kujenga mahusiano mazuri. Jambo la kukumbuka ni kwamba tabia siyo rahisi kufahamika na kuelezeka waziwazi na hasa kama watu wako kwenye mapenzi.Mara nyingi katika mazingira haya sio rahisi kuona kasoro.Vilevile tabia ya mtu huenda ikabadilika na umri.
|
Nifanyeje kuepuka vishawishi vya kujamiiana kutoka kwa watu wengine hasa wakubwa?
Vijana wengi wanajikuta wakitumbukia katika matatizo mazito kama kupata mimba mapema, utoaji wa mimba, magonjwa ya zinaa pamoja na UKIMWI.Kwasababu wanapokea zawadi bila kujiuliza lengo la zawadi hizo.Wanaume wengi wanatumia fedha kuwahadaa wasichana na wasichana wengine wamezoea kupata fedha hizo kukidhi mahitaji yao ya maisha, wanawake pia siku hizi hujaribu kuwahadaa wavulana kwa kuwapatia zawadi ili wakidhi haja zao. Hivyo basi ni muhimu kwa wasichana na wavulana wote kwa pamoja kuwa waangalifu sana na zawadi zinazotolewa.Ni vema wakati wote ujiulize nini lengo la zawadi hiyo.Fikiria kuhusu faida na hasara ya kujamiiana kila unapokutana na vishawishi mbalimbali. Ukikumbuka madhara ambayo unaweza kuyapata itakupa nguvu na msimamo wa kusema “hapana” na kujiepusha na vishawishi.
|
Je, nitahakikisha vipi kwamba urafiki wetu ni wa kudumu?
Hatua ya kwanza ili kudumisha mapenzi kati ya msichana na mvulana ni kujenga msingi mzuri wa mahusiano. Unapochagua rafiki ambaye atakuwa mchumba jaribu kumtafuta kijana ¡V „h mnayeweza kuongea, kujadiliana na kuhojiana kwa uwazi bila kufarakana. „h Mwenye umri unaokaribiana na wa kwako. „h Anayependelea mambo yanayofanana na yale unayoyapendelea. „h Anayeweza kuelewa matatizo yako na yuko tayari kusaidiana nawe kupata ufumbuzi. „h Anayekuheshimu na anayewaheshimu wakubwa zake. „h Unayemwamini. Mahusiano kati yako na rafiki yako wa kike/kiume yanatakiwa kutunzwa na kupaliliwa. Haitoshi kumpata rafiki mzuri halafu ukanyamaza. Unahitaji kuendeleza mawasiliano na majadiliano mbalimbali kama vile kutatua kwa pamoja matatizo yoyote yanayoweza kutokea. Kwa njia hii unaweza kudumisha urafiki wenu.
|
Watu hujamiiana ili kutafuta watoto, nini lengo la kujamiiana iwapo huhitaji watoto?
Ni kweli kwamba mojawapo ya malengo ya kujamiiana ni kutafuta watoto. Lakini si sababu pekee. Sababu hizo ni pamoja na kupata starehe, kujiburudisha, kupoteza mawazo, kujenga na kudumisha mahusiano na hisia za kupendana na kuhitajiana.Hata hivyo ni muhimu sana kuzingatia uzazi wa mpango. Ili kuleta raha katika tendo la kujamiiana na kuzuia mimba isiyotakiwa na kuzaa mtoto ambaye mtashindwa kumlea ni lazima kutumiza uzazi wa mpango. Tumia njia za uzazi kama hamtaki kupata mimba.
|
Nani anayevisha kondom kwenye uume? Mwanamke au mwanaume?
Katika kufanya mapenzi iwe mwanaume anayeweka kondom uumeni au mwanamke anayeshughulika kuweka kondom, itategemeana na makubaliano yao hao wanaohusika.Wote wawili wanaweza kuiweka na pia wote wawili wanaweza kuinunua dukani.
|
Je, nikitumia kondom kila mara ninapojamiiana sitaaambukizwa magonjwa ya zinaa?
Vijidudu vya magonjwa haya vipo ndani ya shahawa.Hivyo ukitumia kondom kila unapojamiiana, siyo rahisi kupata magonjwa ya zinaa, kwa sababu shahawa haipiti kwenye kondom.Kwa hiyo ukitumia kondom kwa njia sahihi, usalama upo.
|
Nifanyeje kujiepusha na vishawishi vya mpenzi wangu vinavyoweza kunifanya nisitumie kondom?
Mara nyingine siyo rahisi kujiepusha na vishawishi vya kujamiiana bila kutumia kondom kutokana na msukumo wa mpenzi wako. Lakini kumbuka kwamba siyo rahisi kutambua mwenye magonjwa ya zinaa na mara nyingi huwezi kujua kama mpenzi wako hana ugonjwa wowote wa zinaa au hata virusi vya UKIMWI. Huwezi kufahamu ni watu wangapi ameshajamiiana nao maishani mwake na mpenzi wako vilevile hawezi kufahamu kama wewe umeshajamiiana na mtu mwingine. Kila unapojamiiana kuna uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa. Kwa hiyo jadiliana na mpenzi wako na mkubaliane juu ya umuhimu wa kutumia kondomu wakati wa kujamiiana kwa nia ya kuwakinga wote wawili. Kama mpenzi wako anakuambia kwamba hana ugonjwa kama huo, mwambie kwamba hana uhakika wa kufahamu kutokuwa na virusi vya UKIMWI bila kupimwa damu. Na kama mmoja kati yenu hajapimwa, basi uwezekano wa kuwa na virusi upo. Usikubali kushawishiwa kutotumia kondom, kwa sababu unaweza kuhatarisha maisha yako.
|
Je, nifanye nini ili wazazi wangu wakubaliane na mimi kuhusu mchumba niliyemchagua?
Mahusiano mazuri na wazazi ni muhimu sana siyo katika masuala ya uchaguzi wa mchumba tu, bali katika masuala yote ya msingi maishani.Kwa hiyo hatua ya kwanza ni kujaribu kuelewana nao. Mara nyingi vijana hufikiri wazazi haelewi maisha ya vijana wa kisasa. Mara nyingine hufikiri kwamba mila na desturi zinamzuia kijana kufanya uamuzi ambao unafaa. Pia wengine hufikiri kwamba tofauti ya malengo kati ya vijana na wazazi huleta migongano. Hali kama hii ikijitokeza ni vizuri kuwasiliana na wazazi kwa nia ya kuelewana.Usisahau kwamba wazazi wakati wote wanajaribu kuboresha hali ya maisha ya watoto wao. Unapowasiliana na wazazi jaribu kuwaeleza kwa heshima na upole kwanini hukubaliani na mawazo yao na kwanini unaona uamuzi wako unafaa. Inawezekana kwa kufanya hivi unaweza ukapata ridhaa ya wazazi wako.Kama hujawahi kuzungumza na wazazi wako kwa karibu mara nyingi inakuwa vigumu kuanzisha mazungumzo. Jaribu kuanza kwa mazungumzo rahisi, tafuta muda mzuri wa kuanzisha mazungumzo.Usianzishe mazungumzo na wazazi wakati wamechoka. Au wakati wametingwa na kazi nyingi hawatakusikiliza. Jaribu kuwa wazi na mkweli na waonyeshe wazazi wako wanaweza kukuamini na kuafikiana na wewe katika maswali mazito zaidi. Onyesha kwamba unawaheshimu. Inachukua muda mrefu kufanikisha mawasiliano mazuri na wazazi lakini ni vema kuyaanzisha mapema kwa ajili ya kufanikisha lengo la mawasiliano mazuri na wazazi.
|
Nikitafuta rafiki kwa nia ya kuoana (mchumba) niangalie sifa gani?
Kuchagua mchumba ni moja ya maamuzi ambayo kijana anahitaji kuyafanya kwa uangalifu mkubwa sana. Kwasababu huyo ndiye atakayekuwa mwenzi wake wa maisha. Katika kuchagua mchumba kila mtu ana mawazo yake kuhusiana na kilicho muhimu kuzingatiwa. Mara nyingi mhemuko una nguvu zaidi kuliko uamuzi wa kimantiki. Hata hivyo vifuatavyo ni kati ya vigezo ambavyo vinaweza kuangaliwa. „h Chagua mtu ambaye anakuheshimu wewe na watu wazima(wakubwa) „h Chagua mtu unayemwamini „h Chagua mtu unayeweza kuongea naye, kujadiliana na kuhojiana kwa uwazi bila kugombana „h Chagua mtu mwenye umri unaokaribiana na wa kwako „h Chagua mtu mwenye afya nzuri „h Chagua mtu anayependelea vile unavyopendelea „h Chagua mtu ambaye ataelewa matatizo yako na yuko tayari kukusaidia kuyatatua
Wafahamishe wazazi wako mtu uliyemchagua na mtambulishe kwao ili wamfahamu na yeye awafahamu.Wakati huohuo na wewe jaribu kuwafahamu wazazi wake.Usifanye uchumba wa haraka. Pata muda wa kutosha kumwelewa rafiki yako.
|