Logo
Sera ya Lugha kiengerezi

Zaidi
Haki na Wajibu wako
Ufanye nini
Uende wapi
 Maswali na Majibu
Chagua Lugha
Kuingia katika majadiliano

 
   
   Hujaandikishwa?
   Andikisha
hapa

   Homepage > Ujinsia > Mimba > Maswali na Majibu
Maswali na Majibu

Chagua swali hapa chini kuona jibu lake!

Je, msichana akijamiiana mara moja tu anaweza akapata mimba?
Je, msichana anaweza akapata mimba kabla ya kuvunja ungo?
Ninaweza kupata mimba wakati nipo kwenye hedhi?
Je,kuna njia salama ya kutoa mimba?
Je, kwa nini inatokea kuzaa mtoto mlemavu?
Je, msichana anaweza kutopata mimba akijamiiana wakati wa siku salama?
Wakati wa kutunga mimba ni mbegu moja tu ya kiume inayopenya kwenye yai, mbegu nyingine zinaenda wapi?
Je, unaweza kupanga kuzaa aina ya watoto, yaani wa kiume au wa kike tu?
Je mapacha wanapatikanaje?
Je, kuharibika kwa mimba kunasababishwa na nini?
Ni siku gani katika mzunguko wa hedhi yai linapoweza kurutunishwa?
Je ni madhara gani atapata mama mjamzito endapo atajamiiana na mwenzi wake?
Dalili za kwanza za msichana au mwanamke kuwa na mimba ni zipi?
Je mwanamke ambaye ana hedhi kila mwezi,anaweza kuwa mgumba?
Ugumba wa mwanaume unasababishwa na nini?
Je mwanaume anaweza akajua kama amempa msichana mimba siku ile ile walipofanya ngono?
Je, mfuko wa maji yanayomzunguka mtoto katika tumbo la mama (yaani chupa) unatoka wapi?
Je, watumiaji wa madawa ya kulevya wanaweza kupata watoto?

Je, msichana akijamiiana mara moja tu anaweza akapata mimba?
Ndiyo, msichana anaweza kupata mimba akijamiiana mara moja tu. Inategemea na mzunguko wa hedhi. Kama ndani ya tumbo la msichana lipo yai pevu ambalo liko tayari kwa kurutubishwana siku ileile msichana anajamiiana anaweza kupata mimba, hata kama ni mara yake ya kwanza kujamiiana.

Je, msichana anaweza akapata mimba kabla ya kuvunja ungo?
Ndiyo. Msichana anaweza kupata mimba kabla ya kuvunja ungo, yaani kabla ya kuona hedhi kwa mara ya kwanza. Hii inatokana na ukweli kwamba kabla ya kuona hedhi, yai ndani ya kokwa linapevuka na kusafiri kutoka kwenye kokwa mpaka tumbo la uzazi.

Hedhi yenyewe ni dalili kwamba lile yai pevu halikurutubishwa na kwa hiyo linatoka pamoja na utando wa tumbo la uzazi kupitia ukeni.
Hii ina maana kuwa hata kama msichana hajavunja ungo na tumboni mwake yai limeshaanza kupevuka, yai hilo linaweza kurutubishwa msichana akijamiiana na kuweza kupata mimba hata kama hajaona hedhi yake kwa mara ya kwanza.

Ninaweza kupata mimba wakati nipo kwenye hedhi?
Ili mwanamke ashike mimba inabidi yai lililopevuka likutane na mbegu za kiume. Yai pevu linapokosa mbegu hufa na kwa vile utando kwenye tumbo la uzazi ulishajiandaa kupokea yai lililorutubishwa hubomoka na pamoja na yai na utando hutoka kama damu ukeni, hedhi.

Hedhi ni dalili kwamba yai halikurutubishwa na hivyo limeshakufa na kutoka. Kwa kawaida, wakati huo halitakuwepo yai jingine lililopevuka kuweza kurutubishwa hivyo uwezekano wa kupata mimba haupo.

Hata hivyo mara chache kuna kosa katika mzunguko wa hedhi na yai jingine linakuwepo tayari kwa kurutubishwa,hata ukiwa kwenye hedhi. Kwa hiyo uwezekano wa kupata mimba wakati wa hedhi upo, hata kama ni mdogo.

Je,kuna njia salama ya kutoa mimba?
Hatari inategemea na mazingira ambapo mimba inatolewa.Kama ni hospitalini na inatolewa na mtaalamu aliyesomea na kama mazingira na vifaa ni safi, uwezekano wa kutoa mimba salama ni mkubwa.Lakini,
hata katika mazingira hayo, shida zinaweza kutokea.

Msingi wa kukumbuka ni kwamba kutoa mimba mwenyewe au hata kwa mtu asiyesomea ni hatari sana. Kwa wanawake wanaojaribu kutoa mimba kuna uwezekano mkubwa wa kupata mambukizi katika via vya uzazi na baadhi yao hutoboa mfuko wa uzazi.Matatizo haya ni hatari sana.

Matatizo yanayohusiana na kutoa mimba ni mazito, kama mfuko wa uzazi kuharibika,mambukizi yasiyotibiwa katika via vya uzazi,kutoa damu nyingi, ugumba au hata kifo kwa mwanamke aliyehusika.

Kwa hiyo ni vizuri zaidi na tena salama kuacha kutoa mimba.Unaweza kuzuia kutoa mimba kwa kuacha kupata mimba isiyotarajiwa, au kwa njia ya kutojamiiana au kutumia njia ya uzazi wa mpango.

Je, kwa nini inatokea kuzaa mtoto mlemavu?
Kuna aina mbalimbali za ulemavu na kuna sababu mbalimbali za kuzaa mtoto mlemavu.Ulemavu wa mtoto unaweza ukatokea katika hatua tatu tofauti, wakati wa utungaji mimba, wakati wa ujauzito na wakati wa kuzaa.
Ili mtoto aweze kutungwa, kuna mlolongo wa mambomengi ambayo yanatakiwa yatokee wakati mwafaka.Ule mwenendo wa kujiunga yai lililopevuka likutane na mbegu ya kiume siyo kitu rahisi na inawezekana yakatokea makosa. Makosa kama hayo siyo rahisi kuyazuia na mara nyingi kutokea kwake ni kwa bahati mbaya.

Sababu mojawapo ni mwanamke kuumwa wakati wa ujauzito. Kama mwanamke mjamzito anaumwa kwa mfano malaria na anakunywa madawa makali, ugonjwa wenyewe au matumizi ya dawa yanaweza kuleta madhara kwa mimba inayokua tumboni. Malaria ni ugonjwa mmojawapo unaosababisha mimba kutoka na ulemavu kwa watoto
wanaozaliwa.

Wanawake wanashauriwa kuwa waangalifu sana wasiugue malaria wakati wa ujauzito. Sababu nyingine ni matumizi ya madawa ya kulevya, pamoja na sigara au pombe wakati wa ujauzito. Vitu hivi sio vizuri kwa mwili wa binadamu,hasa kwa mimba.

Wakati mwingine, ulemavu wa mtoto unatokea wakati wa kuzaliwa.Kwa hiyo ni muhimu sana mwanamke ahakikishe anahudumiwa na mhudumu mwenye ujuzi wa kutosha ambaye anayajua madhara na namna ya kukabiliana nayo.

Je, msichana anaweza kutopata mimba akijamiiana wakati wa siku salama?
Siku salama ni siku ambazo hakuna yai ambalo lipo tayari kwa rutubishwa. Iwapo mwanamke atajamiiana katika siku salama tu wakati ambapo hakuna yai lililo tayari kurutubishwa anaweza asipate mimba.

Hata hivyo kwa vile wasichana wengi mzunguko wa siku zao hubadilika kila wakati, ni vigumu kujua kama kuna yai ambalo lipo tayari kwa kurutubishwa. Kwa hiyo, kuhesabu siku salama siyo njia salama ya kuepuka kupata mimba.

Wakati wa kutunga mimba ni mbegu moja tu ya kiume inayopenya kwenye yai, mbegu nyingine zinaenda wapi?
Ni kweli kwamba wakati wa kujamiiana na kutunga mimba ni mbegu moja tu ya kiume inayopenya kwenye yai. Mbegu zilizosalia hufa na kutoka kupitia ukeni kwa sababu hazina kazi tena. Inashauriwa kwamba watu wanapomaliza kujamiiana, wasafishe vizuri sehemu zao za siri.

Je, unaweza kupanga kuzaa aina ya watoto, yaani wa kiume au wa kike tu?
Mimba inatungwa wakati yai la kike linaporutubishwa na mbegu za kiume. Jinsi ya mtoto inategemea aina ya mbegu za kiume. Nusu ya mbegu za mwanaume zinatengeneza mtoto wa kiume na nusu zinatengeneza mtoto wa kike. Lakini wanaume hawana uwezo wa kuamua aina ya mbegu itakayorutubisha yai. Kwa hiyo, haiwezekani kupanga. Jinsi ya mtoto inategemeana na bahati tu.

Je mapacha wanapatikanaje?
Zipo aina mbili za mapacha, wale wanaofanana na wale wasiofanana. Karibu robo ya mapacha wote hufanana. Hii ina maana kwamba wametokana na yai moja lililotungwa mimba ambalo hujigawa katika makundi mawili tofauti ya chembechembe, kila mojawapo hubadilika kuwa kiumbe pekee. Hadi sasa, wataalam hawaelewi vizuri sababu za yai kujigawa. Mapacha wa aina hii, kwa vile wametokana na yai moja, mara zote huwa na jinsia moja na hufanana sana kimaumbile.

Mapacha wasiofanana hutokea wakati wa yai kupevuka, kokwa za mwanamke hutokea zikawa mayai mawili badala ya moja tu. Mayai yote mawili hurutubishwa na hutungishwa mimba kwa mbegu mbili tofauti za mwanaume. Viumbe viwili hukua wakati mmoja katika mfuko mmoja wa uzazi na kuwa na umri uleule, mapacha hawa ni sawa sawa na watoto wengine wawili wa wazazi haohao. Wanaweza kuwa wa jinsia na maumbile tofauti kabisa.

Je, kuharibika kwa mimba kunasababishwa na nini?
Asilimia 10 hadi 20 ya mimba zinazoharibika huharibika katika kipindi cha wiki 12 za mwanzo wa ujauzito. Sababu kuu hutokana na kuharibika kwa yai lililotungwa mimba. Iwapo yai lingeendelea kukua katika hali hii matokeo ni mtoto kuzaliwa na kasoro mwilini au kiakili. Kwa hiyo mimba kuharibika inaweza kuwa ni njia ya asili ya mwili kukabiliana na matatizo hayo ya kimaumbile.
Vilevile kuharibika kwa mimba huweza kutokea kama mama ana magonjwa kama malaria au kaswende, kama ameanguka chini kwa nguvu au kama ana matatizo katika via vyake vya uzazi. Dalili za mimba kuharibika ni damu kutoka ukeni na maumivu makali ya tumbo kwa chini.

Ni siku gani katika mzunguko wa hedhi yai linapoweza kurutunishwa?
Yai moja hupevuka siku 14 kabla ya hedhi inayofuata. Baada ya yai kukomaa ndani ya kokwa la upande wa kulia au wa kushoto, yai husafirishwa kwenye mrija wa uzazi. Yai likijiunga na mbegu ya kiume ndai ya mrija wa kupitisha mayai siku zilezile, linaweza kurutubishwa. Yaani, endapo mwanamke anajamiiana kipindi cha siku chache kabla yai kupevuka au siku yai linapopevuka anaweza akapata mimba.
Kwa sababu wasichana wengi hawaendi hedhi ya kawaida, yaani mzunguko wa siku 28 katika kila mwezi, ni vigumu sana kwao kufahamu tarehe ya hedhi inayofuata. Hivyo ni vigumu kujua lini litakuwepo yai linalongojea kurutubishwa.
Mzunguko wa hedhi kwa wasichana unaweza kuathiriwa na mfadhaiko, huzuni, safari au mabadiliko mengine katika maisha ya wasichana. Hata kama msichana ana mzunguko wa kawaida wa hedhi hali hiyo inaweza kubadilika ghafla na ukawa sio wa kawaida. Wanawake wengi na hasa wasichana hawawezi kutegemea kuhesabu siku kama njia ya kuzuia mimba, kwa sababu hawezi kuwa na uhakika iwapo lipo yai linalongojea kurutubishwa au la. Hakuna siku salama za kuepukana na mimba!

Je ni madhara gani atapata mama mjamzito endapo atajamiiana na mwenzi wake?
Kama kati ya mwanamke na mwanaume hakuna mwenye magonjwa ya zinaa, hakuna madhara yoyote kwa mwanamke mwenye mimba kujamiiana na mwenzi wake. Mfuko wa mimba hufunga kabisa na chupa inamzunguka mtoto vizuri, na hivyo hakuna uwezekano wowote wa mbegu za kiume kupenya na kumfikia mtoto.
Inashauriwa lakini wakati wa kujamiiana na mwanamke mjamzito tumbo lisigandamizwe sana. Wanawake wengine hawana hamu kubwa ya kujamiiana hasa mwishoni mwa ujauzito, na mwanaume anashauriwa kuheshimu hisia hizi za mwanamke.

Vilevile, kama mwanamke mjamzito anaambukizwa magonjwa ya zinaa wakati wa kujamiiana, inaweza kuwa hatari sana kwa mwanamke na pia kwa mtoto tumboni. Wakijamiiana mume na mke wakati wa ujauzito, lazima awe na uhakika kwamba hamna mwenya magonjwa ya zinaa au watumie kondomu kwa ajili ya kinga. Iwapo watakuwa na wasiwasi wowote, wamwone daktari kwa uchunguzi.

Dalili za kwanza za msichana au mwanamke kuwa na mimba ni zipi?
Dalili moja iliyo wazi zaidi ni kukosa hedhi. Mwanamke akijamiiana na mwanaume bila kutumia kinga yoyote na asipopata hedhi katika muda unaotakiwa, mara nyingi ina maana kwamba amepata mimba.
Dalili nyingine ni kuvimba matiti na chuchu kuchomachoma. Baadhi ya wanawake wanaota mavuzi mengi na wengine wengi rangi ya chuchu inabadilika kuwa nyeusi. Pia, karibu nusu ya wanawake wajawazito huumwa tumbo na wengine hutapika. Wanawake wengi husikia mkojo mara kwa mara na wengine hujisikia wachovu na kuona kizunguzungu, hasa katika miezi mitatu ya mwanzo. Wakati mwingine wanawake hupenda au huchukia baadhi ya vyakula.
Ili mwanamke awe na uhakika kama ni mjamzito au hapana, akapimwe mkojo kwenye kliniki au hospitalini, mara anapokuwa na wasiwasi.

Je mwanamke ambaye ana hedhi kila mwezi,anaweza kuwa mgumba?
Ndiyo, inawezekana kwamba mwanamke anayepata hedhi yake kila mwezi akawa mgumba. Na vilevile inawezekana kwamba mwanamke asiyepata hedhi kila mwenzi siyo mgumba.
Ni kweli kwamba kuna mahusiano fulani kati ya hedhi kila mwezi inamaanisha kuwa mwanamke anao uwezo wa kutengeneza yai kila mwezi. Hata hivyo, siyo rahisi kuwa na uhakika iwapo mirija ya kupitisha yai inaweza kupitisha yai hilo kutoka kwenye kokwa hadi kwenye tumbo la uzazi. Kwahiyo hata mwanamke ambaye anapata hedhi kila mwezi anaweza kuwa mgumba.
Ili mwanamke awe na uhakika kama mgumba au la, ni vyema akamuone daktari kwa ajili ya uchunguzi.

Ugumba wa mwanaume unasababishwa na nini?
Ugumba ni hali ya mwanaume kushindwa kumpa mimba mwanamke. Kuna mambo mengi yanayoweza kusababisha ugumba.
Kati ya wanaume wagumba, wengi wanazaliwa na ugumba na hakuna marekebisho yoyote yanayoweza kufanywa. Katika hali hii, ugumba unasababishwa na kutokamilika kwa via vya uzazi vya mwanaume, mfano kutokuwa na sehemu ya kutengenezea mbegu za kiume au kuwa na shahawa duni. Kwa kuongezeka, kuharibika via vya uzazi kutokana na maradhi, kuziba kwa mirija ya kupitisha mbegu kutokana na magonjwa ya zinaa kama vile kaswende na kisonono. Sababu nyingine za ugumba ni kuwa na uume dhaifu. Hii inaweza kusababishwa na magonjwa ya zinaa, au na mfadhaiko wa kiakili na kisaikolojia. Hali nyingi katika hizi haziwezi kurekebishwa, na zinamsababishia mwanaume kuwa mgumba wa kudumu.
Hata hivyo, pia kuna mambo yanayosababisha ugumba wa muda. Mambo hayo ni pamoja na ugonjwa, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, lishe duni, mshituko na majonzi. Mara zikirekebishwa, mwanaume anarudi hali ya kwa na uwezo wa kumpa mwnamke mimba.

Je mwanaume anaweza akajua kama amempa msichana mimba siku ile ile walipofanya ngono?
Hapana, hamna njia ya kufahamu kama amempa msichana mimba siku ileile wanapojamiiana. Inachukua muda kwa mwili kuonyesha dalili za mimba.
Msichana akitaka kwenda kliniki kupimwa mkojo, kwanza ahesabu tarehe ipi alikuwa anategemea kupata hedhi yake. Kama anakosa hedhi katika muda alioutegemea, itambidi aende kliniki. Mimba inaonekana kwa kupima mkojo wakati ambapo mwanamke alitakiwa kwenda mwezini. Msichana akienda kupimwa mkojo kabla, hali halisi kuhusiana na ujauzito haiwezi kutambuliwa.

Je, mfuko wa maji yanayomzunguka mtoto katika tumbo la mama (yaani chupa) unatoka wapi?
Mfuko wa maji yanayomzunguka mtoto katika mfuko wa uzazi hutengenezwa ndani ya tumbo la uzazi. Hii inatokea mwanzo kabisa wakati wa kutunga mimba, wakati yai linapokutana na mbegu na kurutubishwa. Baada ya kurutubishwa hukaa ndani ya ukuta wa uzazi. Chupa ni mahali ambapo mtoto anatunzwa akiwa tumboni mpaka anapozaliwa. Mfuko wa maji husaidia kumlinda mtoto asipatwe na madhara na misukosuko awapo tumboni.

Je, watumiaji wa madawa ya kulevya wanaweza kupata watoto?
Ndiyo, hii inawezekana. Lakini ujue kwamba watu wanaotumia madawa ya kulevya huwa dhaifu kisaikolojia na kiumbile kwa maana hiyo wanaweza wasiwe katika hali nzuri ya kupata watoto. Hawajali afya zao. Wanakosa hisia na hutumia muda mwingi kushiriki katika matumizi ya madawa ya kulevya; pia hutumia fedha nyingi. Haya si mazingira mazuri ya kulea watoto.