Logo
Sera ya Lugha kiengerezi

Njia
Haki zako
Uende wapi
 Maswali na Majibu
Chagua Lugha
Kuingia katika majadiliano

 
   
   Hujaandikishwa?
   Andikisha
hapa

   Homepage > Ujinsia > Uzuiaji mimba > Maswali na Majibu
Maswali na Majibu

Chagua swali hapa chini kuona jibu lake!

Vidonge na sindano zinazuia mimba kwa kuzuia yai lisipevuke.
Je, ni kweli kwamba ukubwa wa kondomu haufai kwa wanaume wote?
Je, wanawake wanaotumia vidonge au sindano kuzuia mimba wanaweza kupata mimba pindi waachapo mbinu hizo?
Nani anayevalisha kondomu uumeni? Mwanamke au mwanaume?
Je mafuta yaliyopo kwenye kondomu yanaleta madhara yoyote?
Je, mama anayenyonyesha mtoto anaweza kupata mimba?
Kwanini watu wengine wanaamua kutoa mimba?
Je, mapenzi salama ni yapi?
Je, kuna njia ngapi za kuzuia mimba?
Je, mtu aanze kutumia mbinu za uzazi wa mpango akiwa na umri gani?
Je, ni kweli kwamba mwanamke anaweza kupanga uzazi wa mpango akihesabu siku zake?
Je, ni kweli kwamba vidonge vya kuzuia mimba vinasababisha vidonda vya tumbo?
Je, ni lazima kumeza vidonge vya kuzuia mimba siku zote hata zile nisizojamiiana?
Njia gani ya kuzuia mimba inayofaa kwa vijana?
Je kondom ya kiume inatumikaje?
Je, kondom ya kike inatumikaje?
Nani anayevisha kondom kwenye uume? Mwanamke au mwanaume?
Je, ni kweli kwamba ukubwa wa kondom haufai kwa wanaume wote?
Kwa nini kondom itumike mara moja tu?
Kwanini mara nyingine kondom hupasuka wakati wa kujamiiana?
Je, mbegu za kiume zinaweza kupita kwenye kondom?
Je, hayo mafuta kwenye kondom ni ya nini? Yana madhara yoyote?
Je, mwanamke anajisikiaje akijamiiana mwanaume aliyevaa kondom au aliye “peku”?

Vidonge na sindano zinazuia mimba kwa kuzuia yai lisipevuke.
Akitumia njia hizi za kuzuia mimba, mwanamke anaona hedhi yake kama kawaida, lakini hakuna yai linalokuwa limepevuka kwa ajili ya kurutubishwa.


Mara mwanamke akiacha kutumia vidonge, mayai hupevuka tena ndani ya kokwa na mwanamke huweza kupata mimba. Mwanamke aliyetumia sindano, anaweza akachukua muda kiasi kurudia hali yake ya uzazi. Kwa wanawake wengine inachukua miezi 12.

KUMBUKA: sindano na vidonge siyo njia za kudumu za kuzuia mimba, hata kama itachukua muda fulani kurudia hali ya kawaida ya uzazi.

Je, ni kweli kwamba ukubwa wa kondomu haufai kwa wanaume wote?
Kwa wastani ukubwa wa kondomu unafaa kwa wanaume watu wazima karibu wote. Mara chache sana, kondomu ni ndogo kwa wanaume fulani, lakini wakati mwingine wanaume hawataki kutumia kondom kwa kisingizio kuwa wana uume mkubwa hivyo kondom haziwatoshi.

Kwa upande wa vijana, hali ni tofauti. Mara nyingi kondomu ni kubwa sana ukilinganisha na ukubwa wa uume wao. Kutokana na kuwa kwao na uume mdogo, ni vizuri zaidi wangeacha kujamiiana badala yake watumie njia nyingine za kumaliza hamu ya kutaka kujamiiana kama vile kukumbatiana na kubusu.

Je, wanawake wanaotumia vidonge au sindano kuzuia mimba wanaweza kupata mimba pindi waachapo mbinu hizo?
Vidonge na sindano zinazuia mimba kwa kuzuia yai lisipevuke.
Akitumia njia hizi za kuzuia mimba, mwanamke anaona hedhi yake kama kawaida, lakini hakuna yai linalokuwa limepevuka kwa ajili ya kurutubishwa.

Mara mwanamke akiacha kutumia vidonge, mayai hupevuka tena ndani ya kokwa na mwanamke huweza kupata mimba. Mwanamke aliyetumia sindano, anaweza akachukua muda kiasi kurudia hali yake ya uzazi. Kwa wanawake wengine inachukua miezi 12.

KUMBUKA
Sindano na vidonge siyo njia za kudumu za kuzuia mimba

Nani anayevalisha kondomu uumeni? Mwanamke au mwanaume?
Uvalishaji wa kondomu uumeni inategemea makubaliano ya mwanamke na mwanaume wanaotaka kujamiiana. Kwa mantiki hiyo yeyote kati yao anaweza kuuvalisha uume kondomu. Si kuivalisha uumeni tu, wote wawili wanaweza kuinunua dukani.

Je mafuta yaliyopo kwenye kondomu yanaleta madhara yoyote?
Mafuta yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu ni mafuta maalum na kazi yake ni kuhifadhi kondomu mpaka siku yake ya kutumiwa. Bila mafuta haya kondomu isingekuwa imara, ingekauka na isingekuwa nyumbufu vya kutosha. Vilevile mafuta hayo yanalainisha mpira ili kurahisisha uvaaji na matumizi yake. Kwa walio wengi, mafuta haya hayawaletei matatizo yoyote.

Kuna uvumi kwamba mafuta haya yaliyomo ndani ya pakiti ya kondomu yana virusi vya UKIMWI. Hii siyo kweli, mafuta hayo yanawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uimara wa kondomu tu.

Je, mama anayenyonyesha mtoto anaweza kupata mimba?
Katika miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua, mwanamke anayenyonyesha mtoto anapata kinga ya mimba kwa asilimia kubwa. Lakini, inabidi mama anyonyeshe mtoto kwa kipindi kirefu (muda wote mtoto awe ananyonya maziwa ya mama tu na ananyonya kila anapohitaji) na vile vile mama awe hajaanza kupata hedhi yake. Kama mama ameanza kupata hedhi yake au kama anampa mtoto chakula kingine, anaweza kupata mimba tena. Kwa hiyo, anashauriwa kutumia njia za kupanga uzazi ili kuzuia mimba za mfululizo.

Kwanini watu wengine wanaamua kutoa mimba?
Hapa Tanzania utoaji mimba hauruhusiwi kisheria. Hata hivyo watu wengine wanaamua kutoa mimba sababu mimba zao hazikutarajiwa. Kwa mfano msichana mdogo ambaye bado anaenda shule, au mama ambaye tayari ana watoto wengi au umri mkubwa sana. Wanawake wengine wanaamua kutoa mimba kwa sababu wamepata mimba kutokana na kulazimishwa kufanya mapenzi au kubakwa, au kwa sababu baba wa mtoto anakataa kuchukua jukumu la kumlea mtoto. Hizi ni baadhi tu ya sababu za kutoa mimba, na kila mwanamke anayeamua kutoa mimba, ana sababu zake.
Kwa sababu utoaji mimba hauruhusiwi, huduma za kutoa mimba hazipatikani kwa urahisi na wanawake wengi wanajiamulia kutoa mimba wenyewe au kwa msaada wa mtu asiyesomea kufanya hivyo. Kama tulivyosema hapo juu, hii ni hatari sana kwa afya ya mwanamke.

Je, mapenzi salama ni yapi?
Mapenzi salama ni yale yanayofanyika bila ya wasiwasi wa kupata mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Mapenzi salama yanaweza kuwa ni vitendo vya kumaliza hamu za kimapenzi bila sehemu za siri za mwanamke na mwanaume kukutana. Au kama sehemu hizo zinazokutana basi tahadhari inachukuliwa wakati wa kuingiliana kimwili.

Vitendo vya kumaliza hamu bila kujamiiana ni kupiga busu, kukumbatiana, kunyonyana ndimi, kushikana mikono na kupiga punyeto. Matendo haya yote ni salama kabisa kuhusiana na mimba zisizotarajiwa, magonjwa yanayotokana na kujamiiana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Ili kuhakikisha mnafanya mapenzi salama wakati mnahusisha mwingiliano kati ya uume na uke, lazima mchukue tahadhari.Tahadhari mojawapo ni uaminifu katika mapenzi, lakini inabidi muwe na uhakika kwamba wote wawili hamjaambukizwa magonjwa wakati mnapojamiiana kwa mara ya kwanza. Tahadhari nyingine ni kutumia kondom. Kondom inazuia mimba pamoja na magonjwa ya ngono.

Je, kuna njia ngapi za kuzuia mimba?
Njia za uzazi wa mpango zinatofautiana sana na zinaweza kugawanyika katika makundi mengi:

• Vizuizi: hizi huzuia mbegu kulifikia yai. Kuna mipira ya kiume (kondom za kiume) yaani mfuko wa mpira uliozibwa upande mmoja.Unavishwa kwenye uume uliosimama kabla ya kuingia ukeni. Pia kuna mpira wa kike (kondom za kike) yaani mpira unaoingizwa ukeni kabla ya kujamiiana.

• Vidonge vya kuzuia mimba: Lazima mwanamke ameze vidonge hivi kila siku hata kama hajamiiani.
Vilevile kuna njia nyingine za kuzuia mimba kwa muda mrefu. Njia hizi hazihitaji maandalizi maalum kabla ya kujamiiana na pia mwanamke hahitaji kukumbuka kufanya chochote kila siku. Kati ya njia hizi ni pamoja na:

• Sindano: Mwanamke huchomwa hizi kila baada ya miezi mitatu.

• Vipandikizi: Hivi ni vijiti vyembamba vidogo vidogo vinavyowekwa kwenye sehemu ya juu ya mkono wa mama kwa njia ya upasuaji mdogo. Vijiti vina kichocheo kinachozuia kupevuka kwa yai.

• Kitanzi (IUD): Hiki ni kitu kidogo kilichotengenezwa kwa aina maalumu ya plastiki. Kifaa hiki huwekwa kwa utaalamu ndani ya mfuko wa uzazi.

Sindano, vipandikizi na vitanzi ni lazima viwekwe na mtaalamu mwenye ujuzi kwenye kituo cha afya chenye vifaa vya kutosha. Kwa vile dawa za kuzuia mimba kwa muda mrefu zinaingiliana na mzunguko wa kawaida wa hedhi, athari zake ni kubwa kuliko kutumia vidonge.

• Kufunga kizazi: Hii ni njia ya kudumu ya kufunga kizazi. Katika kufanya hili upasuaji mdogo hufanywa. Kwa mwanaume mirija inayopitisha mbegu hukatwa na kufugwa ili kuzuia mbegu zisitoke. Hii inamaanisha kuwa akijamiiana anaweza kumwaga shahawa lakini, ndani ya shahawa hakuna mbegu. Kwa mwanamke mirija ya kupitisha mayai hukatwa na kufungwa, ili kuzuia mayai kufika kwenye mfuko wa uzazi. Baada ya upasuaji huu, mama ataendelea na hedhi kama mwanzo, lakini yai halitaweza kukutana na mbegu za kiume tena.

Vilevile kuna njia nyingine mbalimbali ambazo hazina uhusiano na matumizi ya dawa au vizuizi vya mimba. Njia hizi hazina uhakika mkubwa wa kutopata mimba. Mara nyingine mama anatumia ishara mbalimbali au tarehe kujua lini anaweza kupata mimba, ili kuepuka kujamiiana katika kipindi hicho. Kumwaga mbegu za kiume nje ya uke au kutegemea kwamba mimba hazishiki wakati wa kunyonyesha ni njia nyingine za asili zinazotumika.

KUMBUKA: Njia hizi za asili hutumika sana lakini, si njia salama sana katika kuzuia mimba. Pia njia hizi hazikukingi na maambukizi ya magonjwa ya ngono na VVU. Ni muhimu kupata ushauri kwa wataalamu wa afya kabla ya kuchagua mbinu ya kupanga uzazi

Je, mtu aanze kutumia mbinu za uzazi wa mpango akiwa na umri gani?
Muda unaofaa njia ya kupanga uzazi wa mpango ni unapoanza kujamiiana kwa mara ya kwanza. Huu ni wakati mzuri wa kutumia kondom kwasababu kondom huzuia kupata mimba zisizotarajiwa pamoja na magonjwa ya zinaa.

Huu pia ni muda mzuri wa kwenda kliniki ili kupata ufafanuzi kuhusu ya njia mbalimbali za kuzuia mimba.Daktari au muuguzi anaweza kuwasaidia wanawake na wanaume kuamua njia inayofaa kwa hali yao.

Mara nyingi, watu wanafikiri kwamba huduma ya uzazi wa mpago ni kwa wanawake walioolewa, mama wajawazito na wanawake waliozaa tu. Lakini si kweli. Hapa Tanzania kisheria kila mtu aliyebalehe iwe mvulana au msichana ana haki ya kupata huduma ya uzazi wa mpango.

Je, ni kweli kwamba mwanamke anaweza kupanga uzazi wa mpango akihesabu siku zake?
Yai moja hupevuka na hutoka ndani ya kokwa siku 14 kabla ya kupata hedhi nyingine inayofuata, kwa upande wa kulia au kwa upande wa kushoto. Baada ya hapo, yai hupitia kwenye mirija ya kupitishia mayai mpaka kufikia kwenye mfuko wa uzazi. Iwapo yai litakutana na mbegu ya kiume wakati likisafiri kuelekea kwenye mfuko wa uzazi linaweza kurutubishwa na hivyo mimba kutungwa. Kama mwanamke hatajamiiana kwa kipindi chote cha yai kuwa tayari kurutubishwa anaweza kuzuia kupata mimba.

Hata hivyo wasichana wengi hupata hedhi bila mpangilio na hawafahamu ni tarehe gani watapata hedhi inayofuata. Kwa hiyo ni vigumu sana kujua ni wakati gani yai lipo tayari kurutubishwa. Mzunguko wa hedhi wa msichana unaweza kuathiriwa na huzuni, mfadhaiko, safari au mabadiliko yoyote katika maisha yake. Hata kama msichana alikuwa na mzunguko wa hedhi wenye mpangilio unaweza kubadilika wakati wowote. Kwa hiyo basi wasichana hawawezi kutegemea kuhesabu siku ili kuzuia mimba, kwa vile hawawezi kuwa na uhakika kama yai lipo tayari kwa ajili ya kurutubishwa au la . Hakuna siku salama kwa vijana wa kike.

Je, ni kweli kwamba vidonge vya kuzuia mimba vinasababisha vidonda vya tumbo?
Si kweli. Wanawake wengine wanapata vidonda vya tumbo lakini hivi havihusiani na vidonge vya kuzuia mimba. Vyanzo vya vidonda vya tumbo mara nyingi ni mawazo, mfadhaiko, kula chakula chenye mafuta mengi na viungo vingi. Pia vidonda hivi huhusishwa na familia kuwa na historia ya ugonjwa huu na kamwe vidonge vya kuzuia mimba havisababishi vidonda vya tumbo.

Je, ni lazima kumeza vidonge vya kuzuia mimba siku zote hata zile nisizojamiiana?
Kuna aina ya vidonge inayokuja kwenye pakiti ya vidonge 21 na kuna inayokuja na vidonge 28. Iwapo utapewa ile ya vidonge 21 utapumzika kumeza siku 7 kwa mwezi.Iwapo utapewa ile ya vidonge 28, itakubidi kumeza kidonge kimoja kila siku, hata siku za hedhi.Ili kuhakikisha vidonge vinafanya kazi sawasawa muulize yule aliyekushauri utumie vidonge hivyo jinsi ya kuvitumia.

Kama mwanamke akisahau kumeza kidonge hata kimoja tu, kunauwezekano wa kupata mimba .Anaposahau kumeza vidonge, ni vizuri zaidi wakitumia kondomu wakati wakujamiiana ili kuhakikisha kutopata mimba. Hii inahusisha vilevile kama mwanamke anaharisha au kutapika katika kipindi cha masaa 4 tangu ameze vidonge.

Kama mwanamke anashindwa kukumbuka kunywa vidonge mara kwa mara ni vizuri ushauri kutoka kwa mwenye kliniki ya uzazi wa mpango kutumia njia nyingine ya kuzuia mimba.

Njia gani ya kuzuia mimba inayofaa kwa vijana?
Kila njia ya kuzuia mimba ina faida na hasara zake, kwa mfano faida ya vidonge ni kwamba kama mwanamke atavimeza kila siku, hakuna haja ya kufanya chochote wakati wa kujamiiana. Matatizo ya vidonge ni kwamba mwanamke anahitaji kukumbuka kuvimeza kila siku. Kondom kwa mfano, faida yake ni kwamba, pamoja na kuzuia mimba pia inazuia magonjwa ya zinaa. Kasoro yake ni kwamba unahitaji kuivaa wakati wa kujamiiana.

Vilevile, sindano zina faida kwamba, unachoma mara moja kila baada ya miezi miwili au mitatu kwa kuzuia mimba. Kasoro ya sindano ni kwamba wanawake wengine wanachukua muda mrefu zaidi kurudia hali yao ya uzazi na hupata hedhi bila mpangilio wakati anapotumia sindano.

Kwa hiyo ni jukumu la msichana mhusika na mtaalamu wa uzazi wa mpango kujadili kwa pamoja faida na hasara ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango.Baadaye wanaweza kuamua njia iliyobora zaidi kwa msichana huyo.

Je kondom ya kiume inatumikaje?
Wakati wa kutumia kondomun ya kiume ni muhimu kufuata hatua zifuatazo.Hakikisha kwamba pakiti inayoihifadhi haijapasuka na kwamba tarehe ya kuisha kwa muda wake wa matumizi haijafika.

Kama uume umesimama fungua pakiti kwa uangalifu.Usitumie wembe, meno, mkasi au kisu. Minya sehemu ya juu kutoa hewa ndani ya kondom wakati wa kuivalisha ili kuzuia kupasuka kwa kondom wakati wa kujamiiana.Visha uume kondom taratibu mpaka uufunike uume wote.Ukiwa na uhakika kwamba kondom imevishwa inavyotakiwa unaweza kukutana kimwili na mwanamke.

Wakati wa kutoa uume kutoka ukeni uwe mwangalifu kuhakikisha kwamba kondom bado ipo sehemu inapopaswa kuwa. Baada ya kutoa uume kutoka ukeni, vua kondom kwa uangalifu uume ukiwa bado umedinda ili kuepuka shahawa zisimwagikie ukeni.Tupa kondom iliyotumika kwenye choo cha shimo au ichome moto.Usitupe kondom iliyotumika ovyo.

Ukinunua “salama kondom” ndani ya pakiti kuna maelezo kuhusu matumizi ya kondom.Unapotaka kutumia kondom wakati wa kujamiiana ni vizuri ukajaribisha kwanza ukiwa peke yako ili kuzoea jinsi ya kuitumia.

Je, kondom ya kike inatumikaje?
Kondom ya kike inafahamika kwa jina la “care.”Tanzania hazipatikani sehemu zote na bei yake ni kubwa kidogo. Kondom ya kike huingizwa ukeni kabla ya kujamiiana. Unapotumia kondom ya kike kwanza hakikisha pakiti inayoihifadhi haijapasuka na kwamba muda wake wa matumizi haujaisha.

Chana kwa uangalifu pembezoni mwa pakiti. Kondom ina pete mbili za plastiki na uwazi upande wa juu. Pete moja imelegea ni ndogo na iko kwa ndani, upande usio na uwazi. Pete ya pili ni kubwa, imeshikiliwa na iko upande wa tundu. Shikilia upande uliozibwa na minya pete ya ndani kwa dole gumba, kidole cha pili na cha kati. Mara nyingine inaweza ikakuponyoka endelea kujaribu hadi umeiminya vizuri.Tafuta mkao mzuri na ingiza kondom ya kike ukeni. Huku bado unaminya kwa vidole vyako iongoze kondom ndani ya uke wako. Ukiiachia pete ya ndani itashikilia kondom ndani ya uke .Sasa ingiza kidole chako kwenye kondom sukuma pete mpaka itakapogota kwenye mlango wa uzazi.

Baada ya kujamiiana vua kondom kwa uangalifu. Tupa kondom iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondom iliyotumika ovyo.

Nani anayevisha kondom kwenye uume? Mwanamke au mwanaume?
Katika kufanya mapenzi iwe mwanaume anayeweka kondom uumeni au mwanamke anayeshughulika kuweka kondom, itategemeana na makubaliano yao hao wanaohusika.Wote wawili wanaweza kuiweka na pia wote wawili wanaweza kuinunua dukani.

Je, ni kweli kwamba ukubwa wa kondom haufai kwa wanaume wote?
Duniani kuna kondom za ukubwa mbalimbali.Kwa wastani ukubwa wa kondom unafaa kwa wanaume, watu wazima karibu wote. Mara chache sana kondom ni ndogo kwa wanaume fulani, lakini wakati mwingine wanaume wanaringa tu wakidai kuwa kondom haziwatoshi kwa kuwa wana uume mkubwa. Wengine hutoa kisingizio hicho kwa sababu hawataki kutumia kondom.

Kwa upande wa vijana hali ni tofauti. Mara nyingi kondom ni kubwa sana ukilinganisha na ukubwa wa uume wao. Hapa Tanzania kondom ndogo zaidi kuliko wastani hazipatikani. Kwa vijana pamoja na kuwa na uume mdogo, ni vizuri zaidi wangeacha kujamiiana na badala yake watumie njia nyingine za kumaliza hamu ya kutaka kujamiiana kama vile kukumbatiana na kubusiana.

Kwa nini kondom itumike mara moja tu?
Kondom inapaswa itumike mara moja tu kwa kila mshindo wakati wa kujamiiana, kwa sababu ikitumika mara mbili au tatu uhakika wa kuzuia mimba wala uambukizo wa magonjwa ya zinaa utatoweka. Kondom isifuliwe bali mara baada ya kutumika itupwe kwenye choo cha shimo au ichomwe moto. Kondom zimetengenezwa kwa kutumiwa mara moja tu.

Kwanini mara nyingine kondom hupasuka wakati wa kujamiiana?
Kupasuka kwa kondom mara nyingi kunasababishwa na kondom kutowekwa vizuri uumeni. Ni muhimu sana kutoa hewa ndani ya kondom wakati wa kuivalisha uumeni. Kwa sababu ile hewa uumeni inaweza kusababisha kondom kupasuka wakati wa kujamiiana.

Vilevile sio vizuri kupaka mafuta kama vaselini juu ya kondom ili kurahisisha kitendo cha kujamiiana. Mafuta kama vaselini yanadhoofisha uimara wa kondom na yanarahisisha kondom kupasuka. Mafuta yanayowekwa kwenye kondom yanahifadhi uimara wa kondom na ni aina maalumu ya mafuta.

Ni muhimu kukumbuka kwamba mwanaume akivaa kondom vizuri, uwezekano wa kondom kupasuka ni mdogo sana.

Je, mbegu za kiume zinaweza kupita kwenye kondom?
Hapana, mbegu haziwezi kupita kwenye kondom. Kondom zimetengezwa ili kuzuia mbegu za kiume kufikia ukeni wakati wa kujamiiana. Kwa sababu shahawa haziwezi kupita kwenye kondom. Kondom ni njia nzuri ya kuzuia mimba, maambukizo ya magonjwa ya zinaa pamoja na UKIMWI.

Watu wengine wanasema kwamba kuna mashimo madogo kwenye kondom yanayorahisisha mbegu pamoja na vijidudu vya magonjwa ya zinaa kupita. Huu ni uongo. Ukitaka kuwa na uhakika kwamba kondom mpya haina mashimo, chukua kondom moja ijaze maji. Hayatavuja kabisa. Baada ya kujaribisha itupe kondom ndani ya choo cha shimo au ichome moto, lakini usiitumie wakati wa kujamiana!

Je, hayo mafuta kwenye kondom ni ya nini? Yana madhara yoyote?
Mafuta yanayowekwa kwenye pakiti ya kondom ni mafuta maalum na yana kazi ya kuhifadhi kondomu mpaka siku yake ya kutumika. Bila mafuta haya kondom isingekuwa imara, ingekauka na isingekuwa nyumbufu vya kutoshaVilevile mafuta haya yanalainisha mpira ili kurahisisha uvaaji na matumizi yake. Kwa watu wengi mafuta haya hayawaletei matatizo yoyote. Watu wachache sana ambao ngozi zao ni nyepesi kuathirika wanapata matatizo ya kuwashwa na ngozi baada ya kutumia kondom. Muwasho huo sio wa kudumu. Watu wa namna hii wanashauriwa kunawa na sabuni ya kawaida baada ya kujamiiana.

Kuna uvumi kwamba mafuta yaliyomo ndani ya pakiti ya kondom yana vrusi vya UKIMWI. Hii siyo kweli kabisa, mafuta hayo yanawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uimara wa kondom tu.

Je, mwanamke anajisikiaje akijamiiana mwanaume aliyevaa kondom au aliye “peku”?
Hatuwezi kusema mwanamke husikia raha gani akijamiiana na mwanaume aliyevaa kondom au na mwanaume asiyevaa kondom. Kila mtu ana upendeleo wake, lakini jambo la msingi katika kujamiiana ni hisia, hali ya kuelewana katika mapenzi na kiwango cha msisimko. Wanawake wengine wanapendelea kujamiiana na mwanaume aliyevaa kondom kwa sababu hofu ya kupata mimba au kuambukizwa magonjwa ya zinaa haipo. Wanawake wengine wanapendelea kujamiiana bila kondom. Lakini, pamoja na hatari ya kupata mimba, siku hizi kujamiiana bila kondom kuna hatari ya kuambukizana magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Kwa hiyo ni vizuri zaidi kutomwamini mtu yeyote mpaka mpimwe kliniki wote wawili kuwa ni wazima wa afya.